Native Bible

Psalms 29 · Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version 2015

Listen to Zaburi 29
1Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu. 2Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake. 3Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu. 4Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu. 5Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. 6Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni* urukaruke kama mwana nyati. 7Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi. 8Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi. 9Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” 10Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele. 11Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.

Swahili text and audio: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version™, made available under an open license by Biblica, Inc.