Native Bible

Psalms 27 · Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version 2015

Listen to Zaburi 27
1Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? 2Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. 3Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. 4Jambo moja ninamwomba Bwana, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Bwana na kumtafuta hekaluni mwake. 5Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba. 6Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Bwana na kumsifu. 7Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana, unihurumie na unijibu. 8Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Bwana “Nitautafuta.” 9Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. 10Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, Bwana atanipokea. 11Nifundishe njia yako, Ee Bwana, niongoze katika njia iliyonyooka kwa sababu ya watesi wangu. 12Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. 13Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai. 14Mngojee Bwana, uwe hodari na mwenye moyo mkuu, nawe, umngojee Bwana.

Swahili text and audio: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version™, made available under an open license by Biblica, Inc.