Zaburi 138
Psalms 138 · Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version 2015
1Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote,
mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. 2Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,
nami nitalisifu jina lako
kwa ajili ya upendo wako
na uaminifu,
kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako
juu ya vitu vyote. 3Nilipoita, ulinijibu;
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. 4Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana,
wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. 5Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana,
kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. 6Ingawa Bwana yuko juu,
humwangalia mnyonge,
bali mwenye kiburi
yeye anamjua kutokea mbali. 7Nijapopita katikati ya shida,
wewe unayahifadhi maisha yangu,
unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu,
kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. 8Bwana atatimiza kusudi lake kwangu,
Ee Bwana, upendo wako wadumu milele:
usiziache kazi za mikono yako.
Swahili text and audio: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version™, made available under an open license by Biblica, Inc.